banner

.

.

Thursday, 29 June 2017

DONALD NGOMA ASAINI MKATABA WA MIAKA MIWILI KUICHEZEA YANGA.

HATIMAYE mshambuliaji wa kimataifa wa Yanga, Donald Ngoma  amesaini kuichezea Yanga msimu ujao wa Ligi Kuu ya soka Tanzania bara na kumaliza uvumi kuwa anaenda Simba.
Ngoma aliwaweka roho juu, mashabiki na wanachama wa Yanga kufuatia habari kuwa, angesaini juzi kuichezea Simba kiasi cha Yanga kudaiwa ‘kumteka’ uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere  aliporejea kutoka kwao.
Habari zilizopatikana jana kutoka kwa Kaimu Msemaji wa Yanga, Anderson Chicharito zilisema Ngoma amesaini mkataba wa kuichezea Yanga wa miaka miwili lakini hakutaja dau lake.
Hata hivyo, Ngoma ambaye ni raia wa Zimbabwe amesaini Yanga huku vyombo vya habari nchini Afrika Kusini vikiwa pia vimeripoti amefaulu majaribio na vipimo vya afya kuichezea Polkwane City inayoshiriki Ligi Kuu ya soka ya nchi hiyo.
Chicharito jana alisambaza picha ya Ngoma akionekana na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili Yanga, Hussein Nyika akisaini. Katika picha hiyo, Kiongozi Baraka Desdedit anashuhudia.
Ngoma aliwaweka Yanga roho juu baada ya mchezaji mwingine wa Yanga, kiungo mshambuliaji Haruna Niyonzima wa Rwanda kudaiwa kusajiliwa Simba kwa dola 60,000 ingawa kakanusha.
Wakati Yanga ikimnasa Ngoma, timu ya soka ya Majimaji FC imepanga kusajili wachezaji 11 wapya kuimarisha kikosi chake. Msemaji wa timu hiyo, Zakaria Mtigandi alisema tayari uongozi wao umeanza kufanya mazungumzo na wachezaji wanaotaka kuwasajili na mazungumzo yanaenda vizuri mpaka sasa.
Alisema msimu huu wanahitaji wachezaji 25 badala ya 30 wa msimu uliopita watakaoweza kupambana kuipa timu mafanikio. Alisema wameacha wachezaji 16 na kubakiwa na 14 hivyo hao 11 watafanya kuwa na idadi ya wachezaji 25 wanaohitajika.
Mtigandi aliongeza timu yao haina mpango wa kwenda nje kusaka wachezaji kwani wanaamini wanaweza kupata wachezaji ndani ya nchi na kuifanya timu kuwa ya ushindani. Alisema ili kunyakua wachezaji hao, wameunda kamati ya usajili inayofanya kazi usiku na mchana kupata wachezaji walio bora.

Tupe maoni yako