BEKI mkongwe wa Simba, Method Mwanjali, alikuwa kwenye hatari ya kukatwa katika kikosi kipya lakini mstari mwekundu umempitia pembeni baada ya viongozi wa klabu hiyo kwa kushauriana na madaktari wao kuridhika kuwa hali yake kiafya imeimarika na anaweza kucheza mechi za msimu ujao.
Mwanjali aliumia goti mwanzoni mwa mwaka huu na kushindwa kucheza mechi zote za Ligi Kuu Bara zilizokuwa zimebaki jambo ambalo liliwaogopesha viongozi wa Simba kwamba huenda hadi msimu ujao afya yake itakuwa haijakaa sawa na sasa Mwanjali ameanza kufanya mazoezi yake huko kwao Zimbabwe.
Habari kutoka ndani ya Simba zinasema kuwa kwa sasa usajili ndani ya klabu huo unaelekea ukingoni kwani nafasi muhimu zote zimejazwa ambapo wamesajili wachezaji wanane huku wakiwa bado wanaendelea na mazungumzo na mshambuliaji wa Nkana Rangers ya Zambia, Walter Bwalya.
Simba wameweka jina la Bwalya kwenye mafaili yao huku wakiendelea kupambana naye ili kumshusha kwani anadaiwa kuhitaji pesa nyingi ya usajili pamoja na kulipa gharama za kuvunja mkataba wake na timu yake ambapo inadaiwa ili kukamilisha ni lazima Simba wawe na zaidi ya Dola 100,000.
“Katika usajili huu tumeona Mwanjali abaki, ataongezwa mkataba mfupi ili kuangalia zaidi hali yake, ila madaktari wametueleza kwamba ana uwezo wa kucheza kwani majeraha yake yanaendelea vizuri kwa maana ya kwamba amepona labda itokee vinginevyo,” alisema kiongozi huyo kutoka Kamati ya Usajili.
Simba mpaka sasa imemsajili Emmanuel Okwi, John Bocco, Aishi Manula, Shomari Kapombe, Jamal Mwambeleko, Yusupf Mlipili, Emmanuel Mseja, Ally Shomari, Pius Buswita na Jonas Mkude aliyeongezewa mkataba.
Mwanjali anafikisha idadi ya nyota sita wa kigeni ndani ya Simba pamoja na Laudit Mavugo, James Kotei, Juuko Murshid na Okwi. Simba bado wana nafasi moja ya kujaza ambayo huenda ikajazwa na Haruna Niyonzima ama Bwalya.
Tupe maoni yako