Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Dar es Salaam ambaye pia ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical Ltd cha Dar es Salaam (TPI), Ramadhani Madabida na wenzake watano wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka matano likiwamo la kusambaza dawa bandia na kusababisha hasara ya Sh148.3 milioni.
Wakili wa Serikali, Faraja Nchimbi aliwataja washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo kuwa ni Mkurugenzi wa Operesheni wa TPI, Seif Shamte, Meneja Masoko, Simon Msofe, Mhasibu Msaidizi, Fatma Shango pamoja na wafanyakazi wa Bohari ya Dawa (MSD), Sadick Materu na Evans Mwemezi.
Akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Nyigulile Mwaseba, Wakili wa Serikali, Shadrack Kimaro alisema katika shtaka la kwanza, Aprili 5, 2011, Madabida, Shamte, Msofe na Shango wakiwa na nyadhifa hizo kwenye kiwanda cha TPI walisambaza makopo 7,776 ya dawa bandia za kufubaza virusi vya Ukimwi (ARV) aina ya Antirectroviral.
Tupe maoni yako