Mwenyekiti
wa CCM Mkoa wa Mbeya, Godphrey Zambi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la
Mbozi Mashariki akiwa na katibu wa ccm mkoa wa Mbeya Maganga Sengerema
RAISI wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania,Dk. Jakaya Mrisho Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha
Mapinduzi Taifa anatarajiwa kuwa Mgeni rasmi katika sherehe za maadhimisho ya
Miaka 37 ya kuzaliwa kwa chama hicho zitakazofanyika kitaifa Mkoani Mbeya.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa Habari katika Mkutano uliofanyika katika Ofisi za Chama hicho Mkoa zilizopo
Sokomatola Jijini Mbeya, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya, Godphrey Zambi ambaye
pia ni Mbunge wa Jimbo la Mbozi Mashariki alisema sherehe hizo zinatarajiwa
kufanyika Februari 2, Mwaka huu.
Zambi alisema maadhimisho ya miaka 37 ya
kuzaliwa kwa Chama cha mapinduzi ambayo yatafanyika kitaifa Mkoani Mbeya na
Raisi Kikwete kuwa Mgeni rasmi yataanza majira ya saa 12 alfajiri kwa
kufanya matembezi ya Mshikamano.
Alisema matembezi hayo yataanzia katika
viwanja vya John Mwakangale (nanenane) na kuishia katika Ofisi za Chama Mkoa
eneo la Sokomatola yakihusisha Viongozi wa Chama na Wananchi mbali mbali wa
Mkoa wa Mbeya na mikoa jirani.
Aliongeza kuwa baada ya matembezi hayo
Wananchi na viongozi watapata mapumziko kidogo na kisha kuendelea na sherehe
katika Viwanja vya Kumbu kumbu ya Sokoine zitakazoanza majira ya Saa nane
Mchana.
Aidha mwenyekiti huyo alikipongeza Chama
cha Mapinduzi Taifa kwa kuuteua Mkoa wa Mbeya kuwa Mwenyeji wa Sherehe hizo
ambazo hazijawahi kufanyika Mkoani Mbeya tangu kuzaliwa kwa Chama hicho Mwaka
1977.
Alisema ni fursa pekee ya wakazi wa Mkoa
wa Mbeya ya kukutana na Raisi Kikwete ambaye ataweza kuwaeleza wananchi
mafanikio yaliopatikana Mkoani Mbeya tangu kuzaliwa kwa Chama hicho hadi sasa.
Aliyataja baadhi ya mafanikio kuwa ni
pamoja na Ongezeko la Vyuo vikuu ambavyo awali havikuwepo Mkoani Mbeya sambamba
na kuimarishwa kwa miundombinu hususani ujenzi wa barabara za Lami ambazo
Mbunge wa Chadema Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi anadai yeye ndiye amejenga.
Alisema mafanikio mengine wanayopaswa
kujivunia wakazi wa Mkoa wa Mbeya ni pamoja na sekta ya Elimu, Afya, Maji na
Umeme ambapo sehemu kubwa ya Mkoa wa Mbeya wenye wakazi zaidi ya Milioni Mbili
na Wanachama wa chama hicho zaidi ya Laki tatu wakipata huduma bora za kijamii.
Zambi aliongeza kuwa kutokana na
kufanyika kwa sherehe za maadhimisho ya miaka 37 ya kuzaliwa kwa CCM Mkoani
Mbeya, Mkutano wa Halmashauri Kuu ya Chama hicho ambao awali ulitarajiwa pia
kufanyika Mkoani hapa umeahirishwa na kuhamishiwa mkoa mwingine ambao
haukutajwa.
Wakati huo huo Mwenyekiti huyo
alizungumzia mgogoro unaoendelea ndani ya Chama cha Demokrasia na
Maendeleo(CHADEMA) kwamba CCM haihusika nao kama baadhi ya watu wanavyodai.
Alisema Chama cha Mapinduzi hakifurahii
migogoro ya vyama vya upinzani kwa sababu vilianzishwa kwa lengo la kuikumbusha
Serikali iliyopo madarakani pindi inapofanya vibaya au kujisahau katika kufanya
shughuli za kuwaletea Maendeleo Watanzania.
Alisema hata ndani ya CCM matatizo kama
hayo hutokea lakini humalizwa kupitia vikao halali vya chama na kuendelea na
shughuli zake kama kawaida na sio kukimbilia kwenye vyombo vya habari
kutangaziana mabaya.
Na Mbeya yetu
|