Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema wiki hii itatangaza
tarehe ya uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Kalenga, lililopo wazi baada
ya aliyekuwa Mbunge wake, Dk William Mgimwa (CCM) kufariki dunia
Januari Mosi mwaka huu nchini Afrika Kusini.
Licha ya Kalenga, tume hiyo imesema uchaguzi mdogo pia utafanyika Jimbo la Chalinze baada ya Mbunge wake, Said Bwanamdogo (CCM) kufariki dunia Januari 22 mwaka huu.
Akizungumza ofisini kwake jana, Mkurugenzi wa
Uchaguzi, Julius Malaba alisema uchaguzi mdogo hauwezi kufanyika kama
jimbo litakuwa wazi miezi 12 kabla ya Uchaguzi Mkuu.
“Wabunge hawa wamefariki dunia ikiwa imebaki miezi zaidi ya 12 kabla ya Uchaguzi Mkuu na kuvunjwa kwa Bunge, hilo linamaanisha chaguzi zitafanyika na wiki hii NEC itatangaza tarehe ya uchaguzi jwa Kalenga,” alisema Malaba.
Alifafanua kuwa mbunge anapofariki au vyovyote
vile na jimbo kubaki wazi, NEC inatakiwa kutangaza tarehe ya uchaguzi
ndani ya siku 90.
Malaba alisema daftari la kudumu la wapigakura litakalotumika ni lile lililotumika Uchaguzi Mkuu mwaka 2010.
Katika hatua nyingine, tume hiyo imeeleza kuwa ipo hatua za mwisho za maandalizi ya kuboresha Daftari la Wapigakura.
“Nawahakikishia Watanzania ukifika wakati wa
kupiga kura ya maoni kupata Katiba Mpya, Daftari la Wapigakura litakuwa
limeshafanyiwa maboresho tupo hatua za mwisho na tutaeleza njia ambazo
tutazitumia,” alisema Malaba.
Wakati NEC ikieleza hayo, Shirika la Vijana (TYVA) jana, limeitaka tume hiyo kuhakikisha vijana wote waliotimiza umri wa kupigakura wanaandikishwa katika daftari hilo.
Akizungumza Ofisi za Idara ya Habari (Maelezo),
Mwenyekiti wa shirika hilo, Eric Ahimidiwe alisema kama maboresho hayo
hayatafanyika, ni wazi kuwa vijana wengi watashindwa kupiga kura kupata
Katiba Mpya. “Kuna kundi kubwa la vijana wenye haki ya Kikatiba ya
kupigakura, lakini hawajaandikishwa. Tunaiomba NEC iondoe ukimya na
kutaja siku rasmi,” alisema.
Chanzo: Mwananchi.
Chanzo: Mwananchi.
Tupe maoni yako