Maisha uliyoishi zamani hayawezi kukukwamisha
kufikia malengo uliyojiwekea. Hakuna mtu ambaye alifikiri leo hii Rose Muhando
angeweza kuwa mwanamuziki mkubwa wa nyimbo za Injili anayelipwa fedha nyingi
kutokana na muziki wake, hasa kwa wale waliomjua tangu utoto wake.
Lakini mwanamuziki huyo aliyesaini mkataba wa
miaka mitano na Kampuni ya Sony Music Africa ya Afrika Kusini alioanza
kuutumikia mwaka huu 2014, anasema kuwa maisha yake yalianzia katika hali duni
kwani alikuwa akiombaomba baada ya kufukuzwa katika familia yake huko Dumila
mkoani Morogoro kwa kosa la kubadili dini.
“Nilikuwa mwimbaji mzuri sana wa kaswida,
nilihudhuria kila siku madrasa nikiwa Dumila. Baadaye maisha yangu yalikuwa
magumu sana, chanzo cha haya yote ilikuwa ni ugonjwa uliosababisha afya yangu
kudhoofu. Kwa wakati huo nilipimwa kila ugonjwa sikukutwa na tatizo,
ndipo siku nilipoamua kwenda katika maombi,” anasema Rose Muhando ambaye sasa
anatamba na wimbo Wololo alioutoa chini ya Sony Music Africa.
Anasimulia kuwa baada ya maombi hayo, alipona
na hapo ndipo alipoamua rasmi kubadili dini akiwa na umri wa miaka 12.
“Nilipobadili dini, wazazi wangu walichukizwa
na uamuzi wangu, waliona ni busara kunifukuza nyumbani, kumbe walizidi
kunihatarishia maisha yangu. Niliendelea kutangatanga na baadaye nilipata
waume, ambao walinizalisha watoto watatu,” anasimulia na kuongeza:
“Nikiwa na mtoto wa miezi sita niliwahi
kufukuzwa na mchungaji mmoja jijini Arusha kwa kuwa tu nilikwenda kumwomba
msaada wa fedha kidogo za kurekodi studio. Kitu hicho kiliniuma sana na
sitakisahau katika maisha yangu. Kila nikikaa hukumbuka na kuumia sana.”
Anasema kwamba alifika Arusha kwa ajili ya
kurekodi wimbo wake wa kwanza, ambapo kutokana na kutokuwa na fedha aliona ni
busara kumwomba msaada mchungaji huyo, lakini ilishindikana.
“Alinifukuza nikiwa na mtoto mchanga
aliyekuwa na mgonjwa wa pumu, niliumia sana na hapo ndipo nilipomwambia Mungu
nikasema yeye anajua ameniandalia nini kwenye maisha yangu,” anaeleza Rose.
Anasimulia kuwa alianza safari ya kurejea
nyumbani, lakini kwa bahati nzuri njiani alikutana na watu wenye asili ya
Somalia na kujitambulisha kwao kuwa aliwahi kuwa muumini wa dini ya Kiislamu,
nao walimsaidia na kumsafirisha hadi mkoani Morogoro.
Baada ya kufika Morogoro aliendelea na maisha
na baadaye kujiunga na kwaya moja mjini Dodoma, wakati huo alikuwa tayari na
watoto watatu akiwa pia ameshaokoka.
“Nilianza muziki katika kwaya iliyopo Dodoma,
baadaye nikawa mwalimu wa kwaya hiyo ya Dodoma St. Mary’s katika Kanisa la
Kianglikana la Chimuli. Niliendelea hivyo mpaka nilipoamua kuanza kutunga
nyimbo zangu mwenyewe kwa msaada wa mfuko wa kwaya yetu,” anabainisha na
kuongeza:
“Januari mwaka 2005, ndipo nilipoanza kuona
uwepo wa Mungu, nilipokea tuzo mbalimbali ikiwamo ya MtunziBora wa nyimbo za
Injili, Mwimbaji Bora na Albamu Bora ya Mwaka, zilizotolewa na Tanzania Gospel
Music Awards 2004.”
Tupe maoni yako