banner

.

.

Tuesday, 4 February 2014

MIRATHI YA ASKOFU MOSES KULOLA, FAMILIA YAMEGUKA.

SHETANI ana majaribu yake! Anaendelea kuifuatilia familia ya mtumishi wa Mungu aliyekuwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Evangelist Assemblies of God Tanzania (EAGT), Marehemu Dkt. Moses Kulola.
Habari za karibuni, mpasuko mkubwa umeibuka baada ya kuwepo kwa sintofahamu dhidi ya mirathi ya marehemu huyo aliyefariki dunia Agosti 29, mwaka jana huku makundi mawili yakiibuka.
Awali, Mchungaji Katunzi aliibuka na kudai kuwa yeye ndiye msimamizi wa mirathi ya ambapo tamko hilo lilipingwa na baadhi ya wanafamilia.
Kwa mujibu wa chanzo makini, hivi karibuni Katunzi alitimuliwa nyumbani kwa marehemu Kulola akiwa amepeleka mchele na pesa taslimu shilingi laki tatu (300,000) alizodai ni sadaka kwa mjane wa marehemu.
 
Mchungaji wa Kanisa la EAGT City Center, Florian Katunzi.
“Hivi karibuni Mchungaji Katunzi alikwenda kwa mjane wa marehemu akatimuliwa, walidai ni msaliti mkubwa wa familia.

“Wakati akitimuliwa nyumbani hapo maeneo ya Capripoint, Abel (mtoto wa marehemu) naye alimshambulia mchungaji huyo na kumwambia asirudi tena nyumbani kwa marehemu kwani amekiuka miiko ya uchungaji ya kiapo cha uaminifu,” kilisema chanzo chetu na kuomba hifadhi ya jina.
Pia kiliongeza: “Familia kwa sasa ina mpasuko mkubwa, kuna makundi mawili, wapo wanaomuunga mkono Mchungaji Katunzi na wasiomuunga.

“Kundi linalomuunga mkono linaongozwa na watoto wawili wa marehemu (majina tunayo).
Kundi jingine ni la mjane wa Kulola, Elizabeth Kulola linaundwa na watoto wa marehemu wakiongozwa na Abel aliyekuwa dereva wa marehemu, Mchungaji Dany, Goodluck, Mary, Anna, Janga Faith na Susan.
Mke wa marehemu Moses Kulola.
Mchungaji Dany Kulola kwa sasa yuko Marekani na inasemekana kuwa amechukizwa sana na kitendo cha ndugu wanaomuunga mkono Katunzi.
Marehemu Kulola alikuwa na watoto 13, waliofariki dunia ni Flora, Benjamin na Rachel.
Wosia wa marehemu uliopatikana hivi karibuni unaonesha kuwa, mjane wa marehemu ndiye mrithi halali wa mali zote.

Habari zaidi zinasema Katunzi ameshaitwa na wachungaji wa Kanisa la EAGT ngazi za juu na kumtaka ajitoe katika sakata hilo la mirathi lakini anaendelea kufuatilia.
Habari nyingine kuhusu sakata hilo zinasema kuwa, Jumapili iliyopita akina mama 150 wa Kanisa la EAGT Jimbo la Mwanza walikwenda nyumbani kwa marehemu baada ya kusoma habari kwenye Gazeti la Risasi Jumamosi Toleo Namba 1074 la Januari 25-28, 2014 likiwa na kichwa cha habari; Mgogoro Mzito Mirathi ya Kulola.

Kwa mujibu wa chanzo chetu, akina mama hao walimuombea mjane wa marehemu huku wakimshutumu vikali Katunzi kwa kufanya jaribio la kumpeleka mahakamani mama Kulola kabla ya kufanyika kwa kikao cha ukoo na kuona nani anaweza kuwa msimamizi wa mirathi hiyo.
Mjane wa marehemu alipozungumza na gazeti hili alikuwa na haya ya kusema:
 
“Familia yangu ina mpasuko mkubwa, watoto wangu hawaelewani na Katunzi, nimepata mfadhaiko kuhusu mambo ya familia kuanza kuhusishwa na mahakama, watoto wangu siku hiyo walipomfukuza Katunzi nyumbani niliwagombeza sana kwani halikuwa jambo la kawaida.
“Kwa sasa mambo yote namwachia Mwenyezi Mungu, wote ni watoto wangu siwezi kuwabagua hata siku moja. Kinachosumbua hapa ni kila mmoja kuwa na tamaa ya mali za kidunia. Haya yote ni majaribu ya mwovu shetani.”

Jumatatu iliyopita, saa 2:56- 58 asubuhi, Mchungaji Katunzi hakupokea simu ya mwandishiili kujibu madai ya kuwa aliwahi kutimuliwa na baadhi ya watoto wa mzee Kulola kama chanzo chetu cha habari kilivyodadavua.

Tupe maoni yako