banner

.

.

Thursday, 13 February 2014

Jaji Warioba: Kazi ya Bunge la Katiba siyo kubadili Rasimu.

“Madaraka ya Bunge Maalumu yanakuwa na mipaka endapo Rasimu ya Katiba imeandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba au chombo cha aina hiyo.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema litakuwa jambo lisilo la kawaida kwa Bunge Maalumu la Katiba kubadili hoja ya msingi iliyopo kwenye Rasimu ya Katiba, akisisitiza kuwa jukumu lake ni kuifanyia marekebisho.
Akihutubia mkutano ulioandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), wa tafakuri na maridhiano kuelekea Katiba Mpya jana, Jaji Warioba alisema:
“Madaraka ya Bunge Maalumu yamekuwa yanabadilika kwa kutegemea aina ya mchakato unaotumika. Afrika Kusini, Namibia na Cambodia, Bunge Maalumu lenyewe ndilo lilipewa jukumu la kuandika Rasimu ya Katiba. Katika mazingira haya, Bunge Maalumu lilikuwa na madaraka ya kubadilisha mambo mengi katika Rasimu ya Katiba… lilikuwa na madaraka ya kuachana na Rasimu ya Katiba na kuandika Rasimu Mbadala.
“Madaraka ya Bunge Maalumu yanakuwa na mipaka endapo Rasimu ya Katiba imeandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba au chombo cha aina hiyo.
Bunge Maalumu linaweza kuwa huru kurekebisha baadhi ya masharti yaliyomo kwenye Rasimu ya Katiba lakini si suala la kawaida Bunge Maalumu kubadili hoja ya msingi. Jinsi ushirikishaji wa wananchi unavyokuwa wa wazi na mpana ndivyo madaraka ya Bunge Maalumu yanavyopungua.”

Tupe maoni yako